Kamisheni ya Utalii Zanzibar ni Taasisi inayojitegemea ambayo ipo chini wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale. Kamisheni hii imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria Namba. 6 ya mwaka 2009 na marekebisho yake ya Namba 7 ya mwaka 2012.

Majukumu na Shughuli Kuu za Kamisheni ya Utalii

Kwa mujibu wa masharti ya Sheria hii, majukumu ya Kamisheni ya Utalii ni: -

 1. Kuandaa Sera ya Utalii na Mpango Mkuu (tourism policy and master plan);
 2. Kuendeleza, kuiwezesha na kuitangaza Sekta ya Utalii kuwa na maendeleo endelevu;
 3. Kuitangaza Zanzibar kama kituo na kivutio cha utalii;
 4. Kuutangaza na kuuendeleza utalii wa kiutamaduni na kimazingira;
 5. Kupanga na kuendeleza utalii kwa mujibu wa sera na mikakati ya kimaendeleo ya Serikali;
 6. Kuimarisha na kuratibu sekta za umma na binafsi zinazohusika katika biashara ya utalii;
 7. Kuandaa shughuli ambazo zitasaidia katika kutangaza utalii wa ndani, kikanda na kimataifa
 8. Kusajili, na kutoa vibali (leseni), na kusimamia biashara ya utalii;
 9. Kusikiliza, kufuatilia na kuchunguza malalamiko kuhusiana na biashara ya utalii;
 10. Kufuatilia na kukagua taasisi zinazoendesha biashara ya utalii;
 11. Kuongeza na kuboresha bidhaa za utalii ili kuvutia soko la utalii;
 12. Kusimamia mfumo wa habari wa utalii;
 13. Kufanya utafiti katika Sekta ya Utalii na kuchapisha taarifa zake;
 14. Kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa Sekta ya Utalii kwa uchumi wa taifa na kuwaelimisha majukumu na wajibu wao katika maendeleo ya utalii nchini;
 15. Kuishauri Wizara katika masuala yanayohusiana na maendeleo ya Sekta ya Utalii.

Muundo wa Kamisheni ya Utalii

Kwa mujibu wa marekebisho ya Sheria Namba 7 ya mwaka 2012, muundo wa Kamisheni ya Utalii ni kuwa inaongozwa na Mwenyekiti ambaye anateuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Aidha, kutakuwa na Makamishna wa Utalii. Kiutendaji Kamisheni ya Utalii inaongozwa na Katibu Mtendaji. Aidha, kwa sasa Kamisheni ina Idara mbili (2) ambazo ni Idara ya Masoko na Idara ya Sera, Mipango na Utafiti.

Mawasiliano yetu

Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale
Mnazi Mmoja, Zanzibar.
S.L.P 2277, Zanzibar.
Barua pepe: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
Tovuti: www.utaliismz.go.tz