Matangazo

Matangazo (3)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi akimuapisha Mhe.Lela Mohamed Mussa kuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale katika hafla iliyofanyika leo viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar,kufuatia uteuzi wake baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Octoba mwaka huu

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi amewaapisha Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuwaambia wananchi kazi imeanza na wategemee mafanikio makubwa kutoka Serikalini huku akiwataka Mawaziri kutekeleza mambo 13.

Rais Dk. Hussein Mwinyi aliyasema hayo leo katika hotuba yake huko katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar mara baada ya kuwaapisha Mawaziri aliowateua siku ya Alkhamis ya Novemba 19, 2020.

Mawaziri walioapishwa hivi leo ni, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora (Haroun Ali Suleiman), Waziri wa Fedha na Mipango (Jamal Kassim Ali), Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ (Masoud Ali Mohamed), Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais, Uchumi na Uwekezaji (Mudrik Ramadhan Soraga).

Wengine ni Waziri wa Nchi, Afisi ya Mkamo wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi (Dk. Khalid Salum), Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, (Riziki Pembe Juma), Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali (Simai Mohamed Said), Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo (Tabia Mwita Maulid).

Mawaziri wengine ni Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo (Dk. Soud Nahoda Hassan), Waziri wa Maji na Nishati (Suleiman Masoud Makame), Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi (Abdalla Hussein Kombo), Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi (Rahma Kassim Ali) pamoja na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale (Lela Mohamed Mussa),

Katika hotuba yake Rais Dk. Hussein Mwinyi aliyataja mambo 13 ambayo yanatakiwa kufanywa na Mawaziri hao ikiwa ni pamoja na kwamba kila Waziri ahakikishe anaijua Wizara yake na Taasisi za Wizara husika na kujua muundo wa Wizara na kila taasisi kwa kuitembelea na kujua mafanikio yake pamoja na changamoto zilizopo.

Alieleza haja kwa Mawaziri kutengeneza Mpango kazi wenye bajeti na kuwataka wafanye kwa kutumia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 na kuangalia inasemaje juu ya Wizara zao, hotuba yake ya Baraza la Wawakilishi inaelekeza nini, pamoja na ahadi zake wakati wa Kampeni zinasemaje na kuahidi kupewa vitabu vya ahadi kutoka Afisi yake.

Pamoja na kupata maoni kutoka kwa wadau na kuwambia kwamba kiongozi huwezi kupata mafanikio kwa ufanisi bila ya kupata maoni ya wadau, kwani kazi haiwezekani kufanyika vyema na kutolea mfano Wizara ya Elimu ni kwamba Waziri hawezi kufanya vyema kama hajakutana na Chama cha Walimu.

Alieleza haja ya kufuata Dira ya Maendeleo ambayo iwe ni kigezo katika Mpango kazi wao ambao uwe na bajeti kwani alileza kwamba mpango bila ya bajeti ni rasimu isiyo mpango, na kutaka Mpango utakaoonesha nini kinataka kufanywa na gharama yake.

Rais Mwinyi pia, aliwataka Mawaziri kutembelea miradi yote iliyo chini ya Wizara zao na kujiridhisha kwa kiwango cha ubora wa mradi husika, utaratibu wa zabuni uliotumika, malipo kwa wakandarasi yanavyofanyika na muda wa kukamilisha miradi.

Alitoa mifano miradi aliyoitembelea na kueleza jinsi alivyosikitishwa na mambo yaliyofanyika akitolea mfano Wizara ya Afya katika Hospitali ya Mnazi Mmoja mradi wa jengo la macho, ambapo tayari mkandarasi ameshalipwa fedha zote lakini vifaa havijafika katika sehemu hiyo ya upasuaji wa macho.

Alieleza ziara yake ya bandarini na kujionea jinsi ambapo tayari mkandarasi ameshalipwa lakini ghala limechelewa kwa muda wa miezi mitatu na kupelekea mlundikano wa makontena katika bandari ya Malindi, Zanzibar.

Alisema kuwa hali hiyo iko kila sehemu na kutaka iwe ni mwisho wake leo huku akitolea mfano wa mradi wa kufuga samaki uliopo Beit el ras katika ziara aliyokwenda Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar hapo jana huku akitaka ripoti ya kina, fedha zilizotumika na kwa nini mradi huo uko hivyo.

Pia, alisisitiza uwajibikaji wa wafanyakazi na kuwataka waendelee katika Wizara zao na kutaka kila mfanyakazi anawajibike sambamba na kutaka kujua huduma zinazotolewa kwa wananchi ziwe za uhakika.

Alisema kuwa kuna maeneo mengi watu hawawajibiki na kusema kwamba huduma zinazotarajiwa hazitolewi na kuwataka iwe basi.

Pia, Rais Hussein Mwinyi aliwataka Mawaziri hao kuhakikisha haki za watu zinatolewa, wafanyakazi wanapeta haki zao kama vile posho, fedha za safari pamoja na muda wa ziada ya kazi na kusema kwamba ukati mwengine fedha zinakuwepo lakini anatokea mkubwa mmoja na kusema hamna fedha.

Aidha, aliwataka kusimamia haki za wananchi na kutolea mfano Wizara ya Ardhi na kueleza kwamba watu wananyang’anywa ardhi zao na kuwataka kuondosha malalamiko kwa kuweka mfumo mzuri wa kukutana na wananchi na kuwasikiliza shida zao.

Alisema kwamba amepata taarifa kwamba karibu na uchaguzi yapo maeneo mengi ya ardhi ya wazi yametolewa, hivyo alisisitiza kuwa anataka taarifa ya kina juu ya hali hiyo.

Alieleza suala la utawala bora likiwemo rushwa na kutaka rushwa kuondolewa na kusema ubadhilifu upo na kutolea mfano semina zisokwisha, safari za kikazi zisizo tija, matumizi mabaya ya mafuta na kueleza kwamba hivi karibuni atateua Makatibu Wakuu ili waweze kushirikiana nao katika kuondoa ubadhilifu wa mali.

Akizungumzia suala la wizi, alisema kwamba kuna Wizara zinakusanya lakini fedha hazikusanywi, fedha za bajeti zinaibiwa, fedha zinazopelekwa katika miradi lakini miradi hiyo iko ovyo haitekelezwi na kuwataka hali hiyo iondoke.

Akiyaeleza masuala ya rushwa, ubadhirifu na wizi na kusema Waziri akishindwa kuyashuhulikia hayo inamaana kwamba hawafai na kusisitiza kwamba mkataba waliosaini leo hauna muda na atakaefanya vizuri atabaki na atakaefanya vibaya ataondoka.

Alieleza kwamba amewaahidi wananchi kwamba hatokuwa na huruma wala muhali na kuwaeleza Mawaziri hao kwamba ataanza na wao.

Akieleza jambo la Saba, Rais Dk. Hussein Mwinyi alieleza kwamba ukusanyaji wa mapato ya serikali kwamba zipo Wizara zinatakiwa kukusanya fedha lakini hazikusanyi, na kuitaka Wizara ya Fedha kwenda kuangalia ZRB na TRA, na Wizara ya Ardhi kuna makusanyo ya kodi ya viwanja fedha zinapotea, na kwenye upande wa maliasili na wale wanaopewa vibali vya mchanga kuna rushwa na fedha zinapotea.

Jambo la Nane alilitaja ni kuwa wabunifu na kuwataka kuwa wabufinu kwa kutumia wataalamu watakao kuwa katika Wizara zao na wasingoje mpaka akawaita yeye kwani hakuna Waziri aneweza kusema yeye ni mtaalamu, hivyo ni lazima wabuni njia mpya za kufanya kazi kwa kushirikiana na wataalamu hao.

Kwa upande wa urasimu, alisema kwamba habari ya njoo kesho iwe mwisho sasa kwani watu wanazungushwa sana wengine wanachukua hata miaka wakitafuta huduma na kuwataka kufanya maamuzi kwa maombi wanayoletwa kwao kwani zipo Wizara nyingi hata barua hawajibu.

“Kama jambo linawezekana sema linawezekana na kama haiwezekani sema kama haiwezekani na sababu zangu hizi na wasinyamaze kimywa watu wakaona hawahudumiwi”,alisema Rais Mwinyi.

Aidha, alisema kwamba mambo yenye maslahi ya umma yasicheleweshwe na kama kuna jambo litakaka kufanyika halina maslahi ya umma liamuliwe mara moja kwani muda wao ni miaka mitano na wasikae wakasema watanya mwakani na badala yake waamue.

Wawe wepesi pale pa kubadilisha Sheria kwani zipo changamoto zinazosababishwa na sheria, hivyo ipo haja ya kupeleka mabadiliko ya kubadilisha sheria kama hazikidhi na kutolea mfano udhalilishaji na kueleza kwamba jambo hilo limekuwa ni kilio kikubwa kila sehemu nchini.

Aliwataka kuhakikisha suala la udhalilishaji linaondolewa na kila Waziri anawajibika wa kuangalia sheria na kwa kila chombo kifanye kazi.

Pia, aliwataka kutoa taarifa za kazi zao wanazozifanya kwa kupitia vyombo vya habari nakueleza haja ya kuwa marafiki kwa vyombo vya habari na kuwataka kueleza mafanikio na changamoto zilizopo na kuwataka wawe marafiki na waandishi wa habari na kuwataka wasiwakimbie.

Rais Dk. Mwinyi aliwataka viongozi hao kusikiliza malalamiko ya watu na kutumia njia mbali mbali zikiwemo simu, mitandao ya kijamii, ili wananchi waweze kutoa malamamiko yao na viongozi hao baadae wayatafutie ufumbuzi.

Akieleza jambo la 13, Rais Dk. Hussein alilitaja kuwa ni usafi na kusema kwamba baadhi ya afisi za Wizara ni chafu na kutaka viongozi hao wahakikishe maeneo ya kazi yanakuwa safi na kila jambo walisimamie wao wenyewe.

Alisema kwamba miji ni michafu hivyo, kuna haja ya kusafishwa na kusema kwamba hatokubali kuyaona mambo ambayo anayaona hivi sasa katika miji ya Zanzibar.

Mawasiliano yetu

Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale
Mnazi Mmoja, Zanzibar.
S.L.P 2277, Zanzibar.
Barua pepe: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
Tovuti: www.utaliismz.go.tz